Jengo la Mahakama ya Mombasa. [Picha/ the-star.co.ke]

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mahakama ya Mombasa imetoa agizo la kutiwa mbaroni kwa maafisa wawili wa kituo cha polisi cha Bamburi wanaokabiliwa na shtaka la ufisadi.

Koplo Isaack Ndegwa na Koplo Benson Mutuku wanadaiwa kupokea hongo ya shilingi elfu sabini kutoka kwa Bob Ngome Nyongesa ili kuachilia gari lililokua likizuiliwa na polisi.

Agizo la kukamatwa kwao linajiri baada ya washukiwa hao kukosa kuhudhuria kikao cha mahakama.

Hii ni baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu ya mashtaka ya umma tawi la Mombasa kuwasilisha ombi la kutiwa mbaroni kwa wawili hao.

Naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Alexendra Muteti alisema kuwa wawili hao wamekiuka sheria na sharti watiwe mbaroni.

“Wawili hawa wamekiuka sheria na kudharau mahakama. Sharti watiwe nguvuni na kufikishwa kizimbani,” alisema Muteti.

Hakimu mkuu wa Mahakama ya Mombasa Evance Makori alikubali ombi hilo na kuagiza kukamatwa kwa washukiwa hao.

Wawili hao wanadaiwa kupokea pesa hizo mnamo Machi 24, 2017 katika eneo la fuo ya bahari ya Jomo kenyatta huko Bamburi.