Mahakama ya Mombasa imeagiza kuharakishwa kwa mazishi ya msichana mwenye umri wa miaka 22 aliyefariki mwezi Machi mwaka huu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kesi hiyo inahusisha familia mbili zenye dini tofauti, zilizotofautiana kuhusu vipi marehemu Yasmin Njuguna alivyostahili kuzikwa.

Hii ni baada ya babake wa kambo Issac Njuguna, kudinda kufanyika mazishi ya mwendazake kwa misingi ya dini ya kiislamu.

Hakimu Henry Nyakweba alisema familia ya mama wa marehemu ina haki kikatiba kuzika mwili wa mtoto huyo kwa utaratibu wa kiisilamu wala sio familia ya baba wa kambo.

Siku ya Jumanne, Nyakweba alisema kuwa itakuwa ukandamizaji wa haki iwapo familia ya mama wa mtoto huyo itakosa kumzika mpendwa wao, ikizingatiwa Issac Njuguna ni baba mlezi tu wala si baba mzazi.

Uamuzi huo ulisababisha Issac Njuguna kushikwa na hasira na kutoka katika jengo la mahakama kwa hasira, punde tu baada ya kutolewa uamuzi huo.

Marehemu alifariki akiwa eneo la Mtwapa mnamo Machi 11, 2016 na mwili wake kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali kuu ya ukanda wa Pwani.