Mahakama ya Mombasa imetoa agizo la kutiwa mbaroni kwa mwenyekiti wa kundi la MRC, Omar Mwamnuadzi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Agizo hili linajiri baada ya kiongozi wa MRC kukosa kuhudhuria vikao vya kesi yake.

Siku ya Jumatatu, afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa, kupitia afisa wake Jami Yamina, iliwasilisha ombi la kukamatwa kwa Mwamnuadzi mbele ya Hakimu Daglous Ogoti.

Jami alisema kuwa ni sharti kiongozi huyo kukamatwa, ikizingatiwa amekwepa zaidi ya vikao vitatu vya kesi inayomkabili katika Mahakama ya Mombasa na ile ya Kwale.

“Tunaomba akamatwe na awasilishwe mbele ya mahakama hii,” alisema Jami.

Aidha, mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma alisema kuwa Mwamnuadzi aliwasilisha vyeti bandia vya matibabu kwa kusingizia kuwa alilazwa katika hospitali kuu ya mkoa wa Pwani.

Hakimu mkuu Daglous Ogoti alikubali ombi hilo na kuagiza kiongozi huyo wa MRC kutiwa mbaroni.

Mwamnuadzi amekosa vikao zaidi ya vitatu vya kesi anayokabiliwa nayo ya kuwa mwanachama wa kundi la MRC na kuandaa mikutano kinyume cha sheria.

Kesi hiyo itatajwa Agosti 30, mwaka huu.