Jengo la Mahakama ya Mombasa. Washukiwa hao walitiwa siku ya Jumamosi katika eneo la Kizingo, Mombasa. Picha/ nation.co.ke

Share news tips with us here at Hivisasa

Mahakama ya Shanzu imeagiza watu wanne wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la ISIS kusalia korokoroni kwa muda wa siku 21.

Hii ni baada ya upande wa mashtaka kuomba mahakama muda wa siku 30 kukamilisha uchunguzi wao.

Nasra Faiz Hyder, Salim Mohammed Rashid, Aisha Faiz Hyder na Fatuma Mohammed Rashid walitiwa mbaroni siku ya Jumamosi juma lililopita, katika eneo la Kizingo, Mombasa.

Wakili wa upande wa mashtaka Berly Marinda alisema kuwa wanahitaji muda zaidi kufanyia uchunguzi vipatakalishi, laini za simu pamoja na simu za rununu zilizonaswa na washukiwa hao.

Upande wa mashtaka ulieleza mahakama kuwa Nasra Faiz Hyder na Salim Mohammed Rashid walikamatwa katika mpaka wa Uturuki na Syria na kuregeshwa humu nchini.

Akitoa uamuzi huo siku ya Jumatatu, Hakimu Diana Mochache alisema kwamba kesi za ugaidi zinahitaji muda zaidi wa uchunguzi, na kuagizwa washukiwa hao kuzuiliwa wa siku 21.

Kesi hiyo itatajwa tarehe Machi 13.