Mahakama ya Shanzu imebadilisha uamuzi wa kumuachilia kwa dhamana Haniya Saggar, mke wa marehemu Sheikh Aboud Rogo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akitoa uamuzi huo siku ya Alhamisi, Hakimu Diana Mochache aliagiza Saggar kukaa korokoroni kwa muda wa siku nane.

Haya yalijiri muda mchache tu baada ya Hakimu Mochache kuagiza Saggar kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja.

Katika uamuzi huo wa kwanza, Hakimu Mochache alisema kuwa mshukiwa huyo hawezi kutoroka ikizingatiwa ana watoto wanao mtegemea.

Mochache alibadilisha uamuzi huo baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma kuwasilisha ombi la kusitisha dhamana hiyo.

Mochache alisema amechukuwa uamuzi huo baada ya naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Alexandra Muteti kuwasilisha sababu za kutosha za kusimamisha dhamana hiyo.

Saggar anakabiliwa na shtaka la kukosa kutoa taarifa kwa polisi kuhusu uvamizi wa Kituo cha polisi cha Central.

Wakati huo huo, mahakama imedinda kuwaachilia kwa dhamana Ali Thalili, Luul Ali Thahil na Zamzam Abdi Abdallah walioshtakiwa pamoja na mjane wa Rogo baada ya wakili wao kushindwa kuwasilisha sababu za kutosha.

“Sijaridhishwa na sababu zilizotolewa na wakili Jerad Magolo, na bado kuna mapengo makubwa ambayo mahakama inahitaji kufahamu kabla ya kutoa uamuzi wa dhamana,” alisema Mochache.

Hakimu Diana ameagiza watatu hao kuregeshwa mahakamani tarehe Oktoba 17, baada ya ripoti ya maafisa wa tabia kuwasilishwa mahakamani.

Haniya Saggar, Nastaheno Ali Thalili, Luul Ali Thahil na Zamzam Abdi Abdallah wanadaiwa kukosa kutoa habari kwa polisi kuhusu uvamizi wa kituo cha polisi cha Central.