Mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa amepata pigo baada ya mahakama ya Mombasa kudinda kuhamisha kesi ya ufisadi na utumizi mbaya wa afisi inayomkabili.
Akitoa uamuzi huo siku ya Jumatano, hakimu katika mahakama ya Mombasa, Julius Nang’ea, amesema kuwa mahakama ya Mombasa ina nguvu kikatiba kusikiliza kesi za ufisadi.
Nang’ea ameongeza kuwa sababu zilizowasilishwa na mawakili wa upande wa mashtaka hazina misingi yoyote ya kuishawishi mahakama hiyo kuhamisha kesi hiyo.
Hatua hii inajiri baada ya mbunge huyo na wanakamati wengine 6 kupitia mawakili wao wakiongozwa na Jerad Magolo, kutaka kesi hiyo kuendelea katika mahakama ya Lamu kwa sababu tukio hilo lilitokea katika kaunti ya Lamu.
Mwezi wa Januari, Magolo alisisitiza kuwa kesi hiyo inafaa kusikilizwa katika Mahakama ya Lamu ilikutoa nafasi kwa wakazi wa Lamu kuhudhuria vikao vya kesi hiyo ikizingatiwa wao ndio waathiriwa wakubwa.
Mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa na wanakamati 6 wa hazina ya ustawishaji wa maeneo bunge CDF wanatuhumiwa kutumia vibaya shilingi milioni 1.6 zilizokuwa zimetengewa ujenzi wa kituo cha kutibu mifugo eneo la Witu.
Kesi hiyo itasikilizwa tena Machi 31, 2016 na Aprili 1, 2016.