Aliyekuwa mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa akiwa mahakamani hapo awali. [Picha/ nation.co.ke]
Mahakama ya Mombasa imetupilia mbali ombi la kumuondolea mashtaka ya ufisadi na utumizi mbaya wa afisi aliyekuwa mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa.Akitoa uamuzi huo siku ya Alhamisi, Hakimu Julius Nange’a amesema sharti kesi hiyo iendelee, ikizingatiwa bado shahidi mmoja bado hajatoa ushahidi wake.Hakimu Nange’a amesema kuwa afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma, haikutoa sababu mwafaka za kushinikiza kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo.Hakimu huyo aidha amesema kesi hiyo ni ya ufisadi na utumizi mbaya wa mali ya umma, hivyo basi itakuwa kinyume cha sheria kuitupilia mbali ilhali shahidi mmoja bado anatarajiwa kufika mahakamani.Ombi hilo liliwasilishwa katika Mahakama ya Mombasa na naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa Alexendra Muteti.Muteti alipokea agizo hilo kutoka kwa afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Keriako Tobiko, baada ya kuhisi ushahidi unaozidi kutolewa ni hafifu.Hata hivyo, wakili wa Ndegwa, Jerad Magolo, alipinga ombi hilo na kutaka kesi hiyo iendelee ikizingatiwa inaelekea kumaliza mwaka wa pili tangu ianze.Ndegwa alishtakiwa pamoja na maafisa wengine sita wa kamati ya hazina ya CDF ya eneo bunge la Lamu Magharibi.Wasaba hao wanadaiwa kushirikiana kuiba shilingi milioni mbili kutoka hazina hiyo.