Mahakama ya Mombasa imedinda kutupilia mbali kesi ya ufisadi inayomkabili mwakilishi wa Wadi ya Shanzu Maimuna Salim.

Share news tips with us here at Hivisasa

Salim anadaiwa kupokea hongo ya shilingi laki tano kutoka kwa Leah Aketch, ili kumsaidia kutatua mzozo wa ardhi baina ya yake na serikali ya Kaunti ya Mombasa mnamo Julai mwaka jana.

Hakimu mkuu Teresia Matheka amesema hawezi kutupilia mbali kesi hiyo, kwa sababu visa vya ufisadi vimezidi nchini, huku idara ya mahakama ilikilaumiwa kwa kutoshughulikia kesi hizo.

Hakimu Matheka ameitaka afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma pamoja na tume ya kukabiliana na ufisadi EACC, kuhakikisha kesi hiyo inaendeshwa kwa haraka.

“Mahakama iko tayari kumaliza ufisadi lakini afisi ya mwendesha mashtaka pamoja na tume ya EACC zinajikokota katika kumaliza kesi hizi,” alisema Matheka.

Mwezi uliopita, Bi Aketch aliwasilisha ombi la kuondoa kesi hiyo mahakamani baada ya kutishiwa maisha.

Aketch aliambia mahakama kuwa anahofia maisha yake na kusisitiza kuwa ni bora aondoe kesi hiyo mahakamani.

“Maisha yangu yako hatarini kutokana na kesi hii. Naomba iondolewe niweze kuwa huru kutokana na vitish,” alisema Aketch.

Aliongeza kuwa amekuwa akipigiwa simu na kupokea jumbe fupi za kumtishia maisha.

“Nilipiga ripoti kwa afisi zote husika lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kufikia sasa,” alisema Aketch.