Mahakama ya Mombasa imedinda kutumika kwa ripoti zilizoandikishwa na washtakiwa wa ulanguzi wa pembe za ndovu kama ushahidi wa kesi inayowakabili.
Uamuzi huu unajiri baada ya naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa Alexendra Muteti, kuwasilisha ombi mbele ya Hakimu Diana Mochache la kutaka kutumika kwa ripoti hizo za washtakiwa Ghalib Kara na Abdul Omar kama ushahidi kwa kesi hiyo.
Hatua hiyo ilipingwa na mawakili wa washtakiwa wakiongozwa na Pascal Nabwana, kwa kusema kuwa hatua hiyo ni ukuikaji wa haki za wateja wao na katiba kwa ujumla.
Akitoa uamuzi huo siku ya Jumatano, Hakimu Mochache alisema kuwa kutumika kwa ripoti hizo itakuwa kinyume cha sheria na katiba ya nchi ikizingatiwa ripoti hizo ziliandikishwa kinyume cha sheria kwani ziliandikishwa na afisa wa cheo cha chini.
Mochache alisema kuwa ripoti hizo zingetumika iwapo zingeandikishwa na inspekta mkuu wa polisi, hakimu ama jaji kwa mujibu wa katiba.
Aidha, ameongeza kuwa itakuwa ukiukaji wa haki za washukiwa hao iwapo ripoti hizo zingetumika kwenye kesi hiyo.
Kesi hiyo inamkabili mshukiwa mkuu wa ulanguzi wa pembe za ndovu Feisal Mohamed Ali, Ghalib Kara, Abdul Omar, Pravez Mohamed na Abdulmajeed Ibrahim, wote wakiwa wanakabiliwa na ulanguzi wa pembe 314 zenye thamani ya shilingi milioni 44.