Gavana wa Mombasa Hassan Joho na aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar wakiwa mahakamani hapo awali. [Picha/ nation.co.ke]

Share news tips with us here at Hivisasa

Mahakama ya Mombasa imedinda kwa mara ya pili kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho.Hii ni baada ya aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar kuwasilisha ombi kutaka kuondoa kesi hiyo kwa madai kuwa hana imani na jaji anayesikiliza kesi hiyo, Lydia Achode.Akitoa uamuzi huo siku ya Ijumaa, Jaji Achode alisema kuwa ombi la Omar halina msingi wowote wa maana na kusema kuwa mahakama haina upendeleo kama inavyodaiwa.Jaji huyo alisema kuwa hakuna umuhimu wa kutupilia mbali kesi hiyo ikizingatiwa mashahidi wote wameshatoa ushahidi wao na kesi hiyo inaelekea kutamatika.Omar alidai kuwa Jaji Achode anapendelea upande wa Joho, baada ya wakili wake Yusuf Aboubakar kunyimwa fursa ya kumuhoji Joho kuhusu vyeti vyake vya chuo kikuu.Omar aidha alidai kuwa hakujakuwa na uwazi na usawa katika kusikilizwa kwa kesi hiyo tangu ianze.Hatua ya Omar inajiri baada ya jaji Achode kudinda kujiondoa kwenye kesi hiyo, baada ya kudaiwa kuwa anapendelea upande mmoja.Joho kupitia wakili wake Mohammed Balala alipinga kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo na kuitaka isikilizwe na kukamilika ili wakaazi wa Mombasa wapate kujua ukweli kuhusu madai ya wizi wa kura yaliyowasilishwa na Omar.Omar alimaliza katika nafasi ya tatu kwenye uchaguzi huo wa ugavana.