Gavana wa Mombasa Hassan Joho katika hafla ya awali. [Photo/ zipo.co.ke]
Mahakama kuu ya Mombasa imedinda kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho.
Hii ni baada ya Joho kutaka kesi hiyo kutupiliwa mbali kwa sababu haikujumuisha jina la Naibu Gavana William Kingi.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Lydia Achode alisema ombi la kutaka kutupilia mbali kesi hiyo halina msingi wowote wa kisheria.
Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar.
Omar alishindwa kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 8 baada ya kupata kura 44,000 huku Joho akiibuka mshindi na kura 220,000.
Joho, kupitia mawakili wake wakiongozwa na Mohamed Balala aliwasilisha ombi la kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo kwa madai kuwa haina msingi wowote wa maana ikizingatiwa alichaguliwa kihalali.
Kwa upande wake, wakili wa Omar, Yusuf Aboubakar, aliitaka mahakama kutotupilia mbali kesi hiyo akisema kuwa ombi lililowasilishwa na Joho halina msingi wowote.