Mahakama ya juu siku ya Jumanne ilimzua Waziri wa Usalama wa Ndani Joseph Nkaissery dhidi ya kumtia mbaroni Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho kwa kudinda kurejesha bunduki anayomiliki kwa idara ya usalama.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hapo awali, Waziri Nkaissery alimuonya Gavana Joho kuwa angetiwa nguvuni kama angekosa kurejesha bunduki hiyo lakini katika uamuzi wake, Jaji wa mahakama kuu George Odunga alisema kuwa waziri huyo hana uwezo wa kisheria kumkamata wala kumpokonya Joho bunduki.

Katika rufaa iliyowasilishwa na Seneta wa Siaya James Orengo kwa niaba ya Gavana Joho, Odunga alisema kuwa uwezo wa kusurutisha yeyote anaye miliki bunduki kihalali upo mikononi mwa idara ya kutoa leseni ya kumiliki bunduki na wala sio kwa waziri.

Kwa upande wake, kinara wa Cord Raila Odinga aliyeandamana na Joho wakati wa kesi hiyo alimtaka Waziri Nkaissery kukoma kujiingiza katika siasa na badala yake kuhudumia wananchi kwa usawa.

Hata hivyo, wanasiasa wanaougemea mrengo wa Jubilee wakiongozwa na mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro walimtaka Gavana Joho kusalimisha bunduki hiyo kwa idara ya usalama.

Kesi hiyo itasikizwa tarehe nane mwezi Aprili mwaka huu.