Jengo la Mahakama ya Mombasa. [Picha/ the-star.co.ke]

Share news tips with us here at Hivisasa

Mahakama kuu ya Mombasa imetakiwa kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Aisha Hussein Mohammed.Ombi hilo limewasilishwa mahakamani na wakili wa Mohammed, Bwana Paul Butti.Butti aliiambia mahakama siku ya Jumanne kuwa kesi hiyo haijatimiza vigezo muhimu vya kesi za uchaguzi kwa mujibu wa katiba.“Kesi hii imekiuka vigezo vingi vya kesi za uchaguzi hivyo basi yafaa kutupiliwa mbali,” alisema Butti.Wakili huyo alisema kuwa kesi hiyo inafaa kutupiliwa mbali kwa sababu haina sahihi ya mlalamishi, ambayo ni moja wapo ya kanuni ya kesi za uchaguzi.“Hakuna sahihi ya mlalamishi Saad Yusuf Saad, hatua inayokiuka vigezo vya kesi za uchaguzi,” alisema Butti.Butti aidha alisema kuwa kesi hiyo haijaweka wazi kura alizopata kila mgombea aliyeshiriki katika uchaguzi huo wa Agosti 8.“Hatuajaelezewa idadi ya kura alizopata kila mgombea wa kiti cha uwakilishi Kaunti ya Mombasa, hatua inayokiuka sheria za kesi za uchaguzi,” alisema Butti.Hata hivyo, Mwaniki Gitai, wakili anayemwakilisha mlalamishi Saad Yusfu Saad aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo imetimiza vigezo vyote vinavyohitajika kwenye kesi za uchaguzi, kinyume na inavyodaiwa na Butti.Mwaniki ameitaka mahakama kutupilia mbali ombi hilo na kumtaka Jaji Mugure Thande kusikiliza kesi hiyo ili haki ipatikane kwa mteja wake.Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na mpiga kura Saad Yusuf Saad aliyepinga ushindi wa Mohammed, kwa madai kuwa uchaguzi huo haukuwa wa haki na uwazi.Jaji Thande atatoa uamuzi wake tarehe Novemba 10, 2017.