Raia wa Pakstani waliokamatwa jijini Mombasa. [Picha/ Osman Suleiman].

Share news tips with us here at Hivisasa

Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa imewasilisha ombi la kutaka kuzuiliwa korokoroni raia kumi wa Pakistani kwa muda wa siku 10 zaidi hadi uchunguzi utakapomalizika.Ombi hilo liliwasilishwa mbele ya Hakimu Juliet Kassam na naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka tawi la Mombasa Alexendra Muteti.Muteti anataka washukiwa hao kuziliwa korokoroni ili kutoa fursa kwa maafisa wa usalama kukamilisha uchunguzi wao.“Tunataka muda zaidi maafisa wa upelelezi wamalize uchunguzi wao kabla ya kufunguliwa mashtaka kwa washukiwa hao,” alisema Muteti.Muteti alisema kuwa muda huo utawapa fursa ya kubaini iwapo washukiwa hao wamekuwa humu nchini kwa zaidi ya miaka minne.“Kuna tetesi kuwa washukiwa hawa wamekaa kwa muda wa miaka minne humu nchini na tunataka kuchunguza iwapo ni ukweli,” alisema Muteti.Aidha, Muteti alisema kuwa uchunguzi huo utabaini iwapo washukiwa hao wamekuwa wakifanya biashara mbali mbali bila vibali mwafaka.Alisema kuwa uchunguzi huo aidha utaweka wazi iwapo washukiwa hao wamekuwa wakikwepa kulipa ushuru kwa taifa la Kenya.Mahakama itatoa uamuzi wake siku ya Ijumaa.Raia hao walitiwa mbaroni siku ya Jumatano katika maeneo tofauti jijini Mombasa.Aidha, wanakabiliwa na madai ya kuendesha biashara haramu humu nchini.Kamanda mkuu wa polisi Kaunti ya Mombasa Johnstone Ipara alisema raia hao watafikishwa mahakamani ili kufunguliwa mashtaka.Ipara alisema kuwa washukiwa hao wamekuwa humu nchini kwa zaidi ya miaka minne bila vibali.“Hawa jamaa wamekuwa humu nchini kinyume cha sheria kwa zaidi ya miaka minne,” alisema Ipara.Mkuu huyo wa polisi aliitaja hatua hiyo kama ukiukaji wa sheria kwani wamekuwa wakifanya biashara pasi kutoa ushuru kwa taifa.