Baadhi ya washukiwa hao tisa wa ulanguzi wa dawa za kulevya wakiwa mahakamani mnamo July 31, 2014. [Picha/ nation.co.ke]
Mahakama ya Mombasa imetakiwa kutupilia mbali kesi ya ulanguzi wa dawa za kulevya inayowakabili raia tisa wa kigeni walionaswa kwenye meli ya MV Darya.Kesi hiyo inawakabili raia tisa wa kigeni kutoka Pakistan na India, na watatu kutoka Kenya, wanaodaiwa kunaswa na dawa za kulevya bandarini Mombasa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 mwaka wa 2014.Mawakili wa washukiwa hao wakiongozwa na wakili Jerad Magolo wameiambia mahakama kuwa kesi hiyo inafaa kutupiliwa mbali na wateja wake kuachiliwa huru, ikizingatiwa kuwa meli ya MV Darya ambayo ilikuwa miongoni mwa ushahidi, ilizamishwa baharini kinyume na agizo la mahakama.Magolo alisema kuwa meli hiyo haikuwa na dawa za kulevya na kuyataja madai hayo kama ukiukaji wa haki za wateja wake.“Meli ya MV Darya haikuwa na dawa za kulevya kama ilivyodaiwa na mashahidi waliotoa ushahidi wao mahakamani. Kesi hii inastahili kutupiliwa mbali,” alisema Magolo.Hatua hiyo imepingwa na naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Alexedra Muteti aliyesema kuwa sharti washukiwa hao kuadhibiwa kisheria.Itakumbukwa kuwa meli hiyo ilizamishwa baharini na serikali mwezi Agosti 29, 2014 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa agizo la kuchomwa kwa meli hiyo.Mtafiti kutoka maabara ya serikali Joram Wambua aliambia mahakama hapo awali kuwa waligundua madini ya gypsum walipofanya utafiti wa chemikali zilizopatikana ndani ya meli hiyo.Wambua alisema kuwa hana ufahamu kuwa meli hiyo ilikuwa na heroini.Kwa upande wake, Gulam Karima aliambia mahakama kuwa aliona mifuko ya simiti ikitolewa kwa meli hiyo wala sio dawa za kulevya kama inavyodaiwa.Mkuu wa polisi wa kituo cha Kilindini Simon Simotwa pia aliiambia mahakama kuwa yeye pamoja na wenzake waliikagua meli hiyo kwa mara ya kwanza iliposhikwa baharini ila hawakuona dawa zozote za kulevya.Kesi hiyo itasikizwa Novemba 9, 2017.