Mke wa marehemu Sheikh Aboud Rogo Haniya Saggar akiwa kizimbani hapo awali. Picha/ the-star.co.ke
Hakimu anayesikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili mke wa marehemu Sheikh Aboud Rogo ameilaumu afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma kwa kujikokota kuendesha kesi hiyo.
Hakimu Diana Mochache ameyasema haya katika Mahakama ya Shanzu, baada ya afisi ya mwendesha mashtaka kukosa kuwasilisha mashahidi wanane ili kutoa ushahidi wao siku ya Jumatano.Hakimu Mochache ametishia kumuondolea Haniya Saggar pamoja na wasichana wanne mashtaka hayo ya ugaidi yanoyowakabili iwapo ushahidi wa kutosha utakosa kuwasilishwa mahakamani.“Nitaitupilia mbali kesi hii na kuwaachilia huru washukiwa wote iwapo hakuna mashahidi watakaoletwa mahakamani,” alisema Hakimu Mochache.Hakimu huyo ameilaumu afisi ya Keriako Tobiko, tawi la Mombasa, kwa kukosa kuendesha kesi hiyo kwa haraka, hatua aliyosema imepelekea haki za Saggar na wasichana hao kukiukwa ikizingatiwa kuwa bado wamo rumande.“Haki za washukiwa zinakiukwa ikizingatiwa wamekaa rumande tangu mwaka jana,” alisema Mochache.Aidha, alisema kuwa ameahirisha kesi hiyo kwa mara ya mwisho na kuagiza mashahidi hao kufika mahakamani tarehe Machi 27, mwaka huu.Saggar, Luul Ali Thahalili, Nastaheno Ali Thahalili na Zamzam Ali Thahalili wanakabiliwa na kesi ya ugaidi kufuatia uvamizi wa kituo cha polisi cha Central mwezi Septemba, mwaka jana.