Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Kwale Zulekha Juma katika hafla ya awali. [Picha/ the-star.co.ke]
Mahakama kuu ya Mombasa imetupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Kwale Zulekha Juma.Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa mahakamani mnamo Oktoba 6, 2017 na mpiga kura Omar Mwakaole ambaye alisema kuwa uchaguzi huo haukuwa wa huru na wa wazi.Akitupilia mbali kesi hiyo siku ya Alhamisi,Jaji Njoki Mwangi alisema kuwa kesi hiyo haijatimiza vigezo muhimu vya kesi za uchaguzi kwa mujibu wa katiba.“Kesi hii haijatimiza kanuni hitajika za kesi za uchaguzi kwa mujibu wa katiba," alisema Mwangi.Jaji huyo aidha alimlaumu Mwakaole kwa kukosa kulipa ada inayohitajika kwenye kesi za uchaguzi kwa mujibu wa katiba.“Mwakaole hakulipa pesa ambayo ingekuwa kama dhamana kwa kesi hii kwa kulingana na sheria za uchaguzi," alisema Mwangi.Jaji Mwangi alisema kuwa Mwamlole alijisahau na kukosa kulipa pesa hizo kwa zaidi ya miezi miwili sasa.“Alijisahau kwa miezi miwili sasa na hajalipa pesa hizo bali alitaka kuongezewa muda," alisema Mwangi.Bi Juma aliibuka mshindi katika uchaguzi wa Agosti 8 kupitia chama cha ODM.