Mahakama ya Mombasa imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa kadhi mkuu nchini Sheikh Hammad Kassim ya kutaka kupinga makamishna wa Wakfu wa Kiislamu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya yanajiri baada ya Sheikh Hammad na wengine kuishtaki afisi ya mkuu wa sheria Githu Muingai kuhusu uteuzi wa makamishna wa Tume ya Wakfu nchini, ambao ni pamoja na Sheikh Juma Ngao, Noor Zubeir, Daktari Mwanakitini Bakari, Nagib Shamsan na Shariff Hussein Ahmed.

Mahakama ya Mombasa iliwaambia makamishna hao waendelee kufanya kazi chini ya wakfu huo ambao umekumbwa na utata kwa muda mrefu, huku waumini wa dini ya Kiislamu wakidai kuwa hawafaidiki na chochote kutoka kwa wakfu huo kando na kufujwa kwa mali.

Mwezi jana, taarifa ziliarifu kuwa makamishna na wafanyakazi wa wakfu huo walikosa kupata mishahara yao kwa takribani miezi saba baada ya mahakama kusitisha utendakazi wa makamishna wapya walioteuliwa.

Wakili wa wakfu huo Aboubakar aliiambia mahakama kuwa tangu kusitishwa kwa utendakazi wa makamishna wapya, wafanyakazi wamekuwa na wakati mgumu kupata mishahara yao.