Mahamaka ya Mombasa imewaachia huru raia wawili wa India waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya ulanguzi ya dawa za kulevya.
Praveen Nair na Vikas Balwan ni kati ya washukiwa 12 waliotiwa mbaroni wakiwa katika meli ya MV Darya iliyodaiwa kupatika na dawa za kulevya. Kesi hiyo inawakabili raia tisa wa kigeni kutoka Pakistan na India, na watatu kutoka Kenya, wanaodaiwa kunaswa na dawa za kulevya bandarini Mombasa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.3.Washukiwa hao wanadaiwa kupatikana na dawa aina ya heroine kati ya Julai 7 na Julai 18 mwaka 2014, bandarini Mombasa.Akitoa uamuzi huo siku ya Jumatano, Hakimu mkuu Julius Nange’a alisema kuwa wawili hao ni wanafunzi waliokuwa wakipokea mafunzo ndani ya meli hiyo, hivyo basi hawana ufahamu wowote kuhusiana na mihadarati inayodaiwa kupatikana kwenye meli hiyo.Hata hivyo, naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa Alexendra Muteti amepinga uamuzi huo na kusema kuwa atakata rufaa kupinga kuachiliwa kwao.“Niko tayari kukata rufaa kupinga kuachiliwa huru kwa wawili hawa. Nitahakikisha wamekabiliwa na mkono wa sheria,” alisema Muteti.Meli ya MV Darya ilizamishwa baharini na serikali mwezi Agosti 29, 2014 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa agizo la kuchomwa kwa meli hiyo.Itakumbukwa kuwa mkuu wa polisi wa kituo cha Kilindini Simon Simotwa aliiambia mahakama kuwa yeye pamoja na wenzake waliikagua meli hiyo kwa mara ya kwanza iliposhikwa baharini wala hawakuona dawa za kulevya.Thomas Mutua, afisa kutoka Idara ya madini Kaunti ya Mombasa, aliambia mahakama kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba kemikali za kutengeneza mbolea wala sio dawa za kulevya.Mwezi Aprili, mtafiti kutoka maabara ya serikali Joram Wambua aliambia mahakama kuwa waligundua madini ya 'gypsum' walipofanya utafiti wa kemikali zilizopatikana ndani ya meli hiyo.