Wizara ya kilimo imesema sehemu kubwa ya mahindi ambayo yanawasilishwa kwa maghala ya bodi ya nafaka na mazao NCPB South Rift imeoza.
Wizara hiyo ilisema hali hiyo inatokana na ukosefu wa ufahamu nashaha kuhusu mbinu bora za kuifadhi mahindi hayo.
Waziri wa kilimo Felix Kosgei alisema hali hiyo huwanyima wakulima fedha zaidi kutoka kwa mahindi yao ambayo wanawasilisha kwa maghala husika.
“Kiwango kikubwa cha mahindi ambayo yameoza,yenye maradhi na kukosa kuafikia usafi unaohitajika katika baadhi ya maeneo ya Kusini mwa Rift Valley ni miongoni mwa changamoto ambayo inawanyima wakulima fedha zaidi kutoka kwa mazao hayo” alisema
Akihutubia wanahabari mjini Eldoret, Kosgei alisema hali hiyo hufanya wakulima wengi kurudishwa nyumbani na mahindi yao.
Kuhusu maandalizi ya msimu wa upanzi mwaka huu waziri Kosgei alisema wizara yake tayari imeaagiza mbolea ya kutosha hivyo basi wakulima hawatakuwa na changamoto ya mara kwa mara ya kuchelewa kufika kwa mbolea msimu wa upanzi.
Hata hivyo waziri huyo alitaka wakulima kutoka North-Rift kuasilisha mahindi yao kwa vituo vya kununulia mahindi karibu nao ili kupunguza msongamano katika mabohari ya Eldoret na Moi’s Bridge.
Kosgei alisema kufikia mwishoni mwa mwezi jana serikali ilikuwa imenunua magunia 1,442,064 ya kilo 50 kutoka kwa wakulima North-Rift kwa kutumia Sh2,239,525,392 kutoka kwa Sh2,824,961,384 ambazo serikali ilitoa kwa ajili ya kununua mahindi kutoka kwa wakulima.