Mbunge wa Nyali Hezron Awiti ameiomba idara ya usalama kufanya uchunguzi dhidi ya watu ambao alisema wamekuwa wakimtishia maisha kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli moja mjini Mombasa, Timothy Odhiambo, mmoja wa walinzi wa Awiti alisema watu wasiojulikana wamekuwa wakimfata mbunge huyo.
“Watu hao wameingia kwenye makazi ya Awiti mara kadhaa, jambo ambalo mbunge mwenyewe amelitaja kama la kuogofya na kutishia maisha yake pamoja na walinzi wake,” alisema Odhiambo.
Awiti aidha amesema ipo haja ya polisi kuimarisha usalama kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa kila mkaazi wa Pwani anaishi bila ya hofu yoyote.
“Singetaka mambo ninayoshuhudia yamkumbe mwananchi yeyote kwa kuwa imekuwa kama desturi kwa watu hao kunivizia,” alisema Awiti.
Hata hivyo, mbunge huyo amewahakikishia wafuasi wake kwamba bado yupo tayari kupambana na Gavana Hassan Joho kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha Ugavana Kaunti ya Mombasa kwenye uchaguzi mkuu ujao.