Baada ya idara ya usalama Pwani kumpokonya Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho walinzi wake watano wa kitengo cha GSU, sasa adai maisha yake yako hatari.
Kulingana na Gavana Joho, huenda mahasidi wake wa kisiasa watakapata nafasi ya kumuandama kwani maafisa aliopewa na serikali wa kitengo cha GSU sasa wamerudishwa kambini kutekeleza shughuli zao za kiusalama katika vitengo vyengine vya kiusalama.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi baada ya kukutana na maafisa wakuu wa idara ya usalama eneo Pwani, Joho alisema kwa sasa anahofia usalama wake.
Joho aidha aliilaumu Serikali kwa kutoliangazia swala hilo akisema kuwa kuna baadhi ya viongozi wakuu wa kisiasa serikalini walitoa agizo hilo la kupokonywa walinzi wake ili kumdhalilisha kukihama chama cha ODM na kujiunga na vyama vyengine vya kisiasa ikiwemo chama cha Jubilee.
Joho alipokonywa walinzi hao baada ya mshirikishi mkuu wa utawala eneo la Pwani Nelson Marwa kudai kuwa walinzi wa Joho, wale wa Amason Kingi wa Kilifi na Aisha Jumwa mwakilishi wa kike wa kaunti ya Kilifi kutumia mamlaka yao vibaya kwa wakaazi wakati wa uchaguzi mdogo wa Malindi siku ya Jumatatu.