Askofu wa jimbo katoliki la Nakuru Maurice Muhatia Makumba sasa anataka majadiliano kufanywa kuhusu shinikizo la upinzani Cord kutaka kuondolewa afisini kwa makamishna wa tume huru ya uchaguzi na mipaka, IEBC.
Kupitia kwa mahojiano katika kaunti ya Nakuru, askofu Muhatia alisisitiza kuwa suluhu la kudumu kuhusiana na tatizo hilo litapatikana tu kupitia kwa njia ya majadiliano.
Askofu huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa tume inayoshughulikia maswala ya elimu na elimu ya kidini katika baraza la maaskofu wa kanisa katoliki hapa nchini, KCCB, aidha alisema katiba ya Kenya inaelezea wazi kuhusiana na njia ambazo zinaweza kutumiwa kuwaondoa makamishna walio afisini kisheria ambazo zinafaa kufuatwa.
‘ Wakati ambapo kunatokea jambo linalotishia kuleta msukosuko katika nchi, ili kuweza kupatikana suluhisho la kudumu, ni muhimu watu wote husika waweze kuja pamoja ili kuweza kusikizana na kuzungumza. Watu wanapozungumza, mambo hulainika,’ alikariri askofu Muhatia .
Ingawa anakiri kuwa wakenya huenda wamepoteza imani katika tume hiyo ya uchaguzi na mipaka, alisema sio vyema kwa makamisha hao kufurushwa kwa lazima kutoka afisini bila ya sheria kuzingatia .
Aidha anasisitiza kuwa ni lazima majadiliano hayo yahusishe wadau wote muhimu kama vile serikali, muungano wa upinzani wa Cord na tume hiyo.
‘ Ni vizuri kwa wanasiasa wa upinzani na watu wa serikali na wahusika wengine kuhusishwa. Maswala ya IEBC hayahusu vyama vya kisiasa pekee. Kuna mwananchi wa kawaida kama mimi na wewe ambao lazima sote tuhusiswe. Pia kuna taasisi zingine ambazo pia zinahusika na mambo ya uchaguzi. Ni vizuri katika kujadiliana hizi taasisi zote na hawa watu wote waje pamoja,’ alisema askofu Muhatia.
Ni matamshi yanayojiri huku IEBC ikisema kuwa itashikilia msimamo wake licha ya kuweko kwa wito wa kujiuzulu kutoka kwa wanasiasa.