Majaji nchini wamelalamikia kuhujumiwa kwa utendakazi wao na baadhi ya viongozi wakuu serikalini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakizungumza siku ya Jumanne katika kongamanao la kila mwaka la majaji mjini Mombasa, majaji hao walisema kuwa wakati mwingine wao hulazimika kutoa uamuzi usioambatana na vipengele vya katiba kufuatia msukumo wa baadhi ya viongozi wakuu serikalini.

Majaji hao walisema kuwa hatua hiyo inakiuka haki na sheria za katiba ya nchi.

Wakiongozwa na anayeshikilia wadhfa wa Jaji mkuu kwa sasa, Jaji Mohamed Ibrahim, majaji hao walisema kuwa idara ya mahakama inafaa kupewa nafasi kuyawajibikia majukumu yake kikamilifu ili kupunguza msongamano wa kesi mahakamani.

"Tunawahimiza viongozi wakuu serikali kutoingilia jukumu la idara ya mahakama ili kuhakikisha maswala mbalimbali ya kisheria na maamuzi ya mahakama yanatekelezwa vyema, hususan wakati huu ambapo taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu,” alisema Ibrahim.

Aidha, alisema kuwa idara ya mahakama lazima ipewe nafasi ya kubadilisha baadhi ya maswala nchini yanayohujumu ugatuzi ili taifa liwe na muongozo mwafaka.

Kongamano hilo lilianza siku ya Jumatatu na litatamatika mwishoni mwa juma hili.