Maafisa wa polisi mjini Mombasa wanaendeleza msako dhidi ya genge la majamabazi linaloshukiwa kumpiga risasi afisa mmoja wa polisi Bomboni mjini Mombasa siku ya Jumapili usiku.
Kulingana na afisa mkuu wa polisi wa kisiwani Mombasa, Martin Asin, tayari maafisa wa polisi wametumwa kila sehemu kuimarisha usalama pamoja na kulisaka genge hilo linaloaminika kuwa hatari.
Akizungumza mjini Mombasa na wanahabari siku ya Jumatatu, Asin alisema kuwa maafisa wa polisi wanashika doria kikamilifu na kamwe hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kuvuruga usalama wa mji huo. Alitoa onyo kali kuwa atakayepatikana atakabiliwa barabara.
“Maafisa wa polisi wako macho na wanashika doria kila sehemu ya mji wa Mombasa. Atakayepatikana akijaribu kuvuruga usalama ataona moto,” alisema Asin.
Aidha alisema kuwa afisa huyo wa polisi alipigwa risasi na kujeruhiwa wakati akishika doria nyakati za usiku. Genge hilo lilitoweka bila kuchukua chochote kwa afisi huyo baada ya kumpiga risasi na kumjeruhi.
“Polisi hawatakubali kujeruhiwa na vijana wadogo hilo halitakubalika lazima usalama umarishwe,” aliongeza Asin.
Hata hivyo, Asin amesema kuwa genge hilo linaaminika kupata mafunzo kutoka kwa kundi la kigaidi la Al Shabab nchini Somalia na kuingia humu nchini ili kuvuruga usalama.