Majambazi wanne walipigwa risasi na kuawa na maafisa wa polisi Jumatano usiku katika kaunti ya Nakuru, huku mmoja was polisi akipata majeraha.
Akidhibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi katika kaunti ya Nakuru, Bernard Kioko alisema kwamba majambazi hao walipigwa risasi na kuawa katika mtaa wa Mwariki katika viunga vya mji wa Nakuru.
“Maafisa wa polisi walipata fununu kutoka kwa mwendeshaji moja wa gari ambaye alitupasha habari juu ya majangiri hao na tukawafuata,” alisema Kioko.
Kioko alisema kwamba majambazi hao waliamurishwa kusimama lakini wakakaidi amri ya maafisa wa polisi ndipo ufiatulianaji mkali wa risasi ulianza.
“Maafisa wetu walifiatuliana risasi na majambazi hao na wakafanikiwa kuwauwa wanne na afisa moja wetu akapata majeraha,” alisema Kioko.
Kioko alisema kwamba afisa aliyejeruhiwa alipelekwa katika hosipitali ya Valley Hospital, ambapo alitibiwa an kuruhusiwa kwende nyumbani.
Afisa huyo alisema walipata bunduki moja gushi, viuma vya kukata nyumba,panga na funguo za magari.
Kioko aliwashukuru wakaazi wa mtaa wa Mwariki na akawahimiza kuendelea kushirikiana na maafisa wa kikosi cha polisi katika juhudi za kuangamiza uhalifu.
Aidha, aliendelea kusema kwamba polisi wataimarisha juhudi zao katika kuimarisha usalama katika kaunti ya Nakuru.
“Maafisa wetu wa polisi wataendelea kudumisha usalama kwa manufaa ya wakaazi wa mji wa Nakuru,” alisema Kioko.