Kaunti ya Mombasa ikiwa miongoni mwa kaunti athirika kwa masuala ya dawa za kulevya, maeneo matatu kwenye kaunti hiyo yametambuliwa kwa kuwa na idadi kubwa ya wauzaji na waathiriwa wa mihadarati.
Kulingana na kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa, kwenye hotuba yake kwa hadhara siku kuu ya Mashujaa mjini Mombasa, maeneo ya Old Town, Majengo na eneo la Tudor miongoni mwa mengine ndiyo yaliyoathirika zaidi.
Alisema kuwa maeneo hayo sharti yaangaziwe, na akaahidi kuweka vita dhidi ya vijana wanaotumia dawa hizo pamoja na walanguzi ambao alitaja kuwa chanzo kikuu cha vijana wengi kutoka kaunti ya Mombasa na eneo zima la pwani kwa ujumla.
Marwa alidokeza kuwa japokuwa wauzaji pamoja na wasambazaji wa mihadarati wameanza kutumia mbinu fiche ili kufanikisha biashara hiyo haramu, bado afisi yake, ile ya idara ya polisi kwa ushirikiano na wananchi na serikali ya kaunti wataendelea kuwaandama washukiwa wakuu wa kuuza mihadarati kwenye kaunti hiyo.
“Maeneo mengi humu katika kaunti yameathirika sana, lakini mitaa kama Majengo, Tudor pamoja na Old Town yana idadi kubwa ya watumiaji na walanguzi, na tutaendelea kuweka juhudi za kupambana na walanguzi wa dawa hizo, na tunaomba wananchi kusaidia katika juhudi hizo,” alisihi kamishna Marwa.
Marwa aidha aliweza kutoa nambari za usajili za magari ambayo yanakisiwa kusambaza dawa hizo za kulevya kwa vijana na watumizi kwenye mitaa hiyo husika pamoja na mitaa mingine ndani ya kisiwa cha Mombasa.