Serikali ya Kaunti ya Mombasa imeimarisha msako wake dhidi ya majengo yaliyojengwa kiholela.
Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mpangilio wa Mji katika Kaunti ya Mombasa Bwana Anthony Njaramba amesema kwamba kitengo cha kukabiliana na majanga na wahandisi wa majengo wanaendeleza ukaguzi wao katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.
Alisema kuwa hatua hiyo inanuia kubaini majengo yaliyoidhinishwa kinyume cha sheria.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Njaramba alisema kwamba matokeo ya ukaguzi huo yatawekwa wazi kwa umma.
Aidha, alisema kuwa wamiliki wa majengo hayo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Njaramba alisema kuwa majengo yote ambayo huenda yakasababisha hatari kwa wakaazi na wafanyibiashara mjini humo yatabomolewa mara moja.
"Tayari ukaguzi wa majengo yaliyojengwa kiholela unaendelea na ripoti itawekwa wazi ili wamiliki wa majengo hayo kuchukuliwa hatua," alisema Njaramba.
Mkuu huyo wa idara ametoa onyo kali kwa maafisa wa serikali ya kaunti hiyo kuwa watakaoshirikiana na wawekezaji walio na tabia za ulaghai kwa kukiuka sheria za ujenzi watakabiliwa kwa mujibu wa sheria.