Wakaazi wa mtaa wa Manyani wamelalamikia kile ambacho wamekitaja kuwa maji ya mvua kufukua miili ya wafu katika makaburi ya Nakuru kusini.
Wakiongozwa na Neto Sakwa wakati walipozuru makaburi hayo, walisema kuwa ukosefu wa miundo msingi kama vile mitaro ya kupitisha maji taka imepelekea maji kutoka mjini kuteremka hadi makaburi hayo ya Manyani.
Waliongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kwamba maji hayo yameanza kusababisha miili ya wafu kufukuliwa na kuwa athari kwa afya ya binadamu.
"Haya maji ya mvua yamekuwa kero sana maanake maji yote kutoka mjini Nakuru yanaishia makaburini hapa Manyani na kufukua miili ya walozikwa," alisema Sakwa.
Ni matamshi yaliyoungwa mkono na Martin Lunalo, mkaazi na kiongozi wa vijana Kivumbini.
Kwa mujibu Lunalo, serikali ya kaunti inafaa kushughulikia swala hilo kwani ni kero na athari kwa afya ya binadamu.
Hata hivyo, afisa wa afya ya umma Nakuru Samuel King'ori katika mahojiano na mwanahabari huyu kuhusiana na swala hilo alisema kuwa serikali imepokea lalama zao na hatua itachukuliwa ili kuepuka athari zaidi.
Itakumbukwa kuwa serikali ya kaunti ya Nakuru ilifunga makaburi ya Nakuru kaskazini na kupelekea shughuli zote za kuzika miili kuelekezwa makaburi ya Manyani.