Wenyeji wa Kaunti ndogo ya Yatta wametoa mwito kwa serikali kuu pamoja na serikali ya Kaunti ya Machakos kuwapa chakula cha msaada.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Maeneo mengi katika kaunti ya Machakos yameangamizwa na ukame ambao umesababishwa  na ukosefu wa mvua katika maeneo mengi ya Kaunti hiyo ikiwemo Yatta, Masinga, Kangundo na Matungulu.

Wakizungumza na wanahabari katika mji wa Matuu siku ya Alhamisi, wakaazi hao waliiomba serikali iwasaidie na chakula cha msaada kwani wameadhiriwa vikali na janga hili.

Walizidi kulalamika kuwa wanafunzi wengi katika shule nyingi sehemu hiyo wamelazimika kubaki manyumbani wakisaidia wazazi kutafuta chakula.

Inasemekana kuwa familia nyingi katika eneo hilo hupata chakula cha jioni peke yake. 

Mary Mutua ambaye ni mkaazi wa kitongoji cha Kateki kilicho katika kaunti ndogo ya Matuu asema kuwa sehemu hiyo imekumbwa na ukosefu wa chakula pamoja na maji hali inayofanya maisha kuwa ngumu.

“Msimu uliopita sehemu nyingi hazikupata mvua ya kutosha jambo ambalo lilisababisha mavuno duni,” asema Mutua.

Wazazi ambao wana watoto shuleni waliiomba serikali kuu kuhakikisha kuwa waalimu katika shule za umma hawaitishi karo katika shule hizo kwani serikali imegharamia masomo hayo.

James Nguku ambaye ni mzazi alisisitiza haya kwa kusema kuwa wazazi wengi huuza mavuno ili kupata karo.

“Kama wazazi tumefinywa na karo ambayo watoto wetu wanaitishwa. Jambo hili litawafanya wengine wetu kushindwa kuwapeleka watoto shuleni,” akasema Nguku.

Wakaazi hao walitaka serikali ianze mfumo wa kupatia watoto chakula hasa katika shule za msingi kwa sababu watoto wengi wamebaki kusalia nyumbani na kukosa elimu kwa sababu ya njaa.