Naibu gavana wa kaunti ya Kisii Joash Maangi amewaomba wafadhili au makanisa ya shule mbalimbali kuwa mbali na usimamizi wa shule ili kuupa usimamizi wa shule husika wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Maangi pia aliwaomba wazazi na viongozi wa kisiasa kutoingiza siasa katika shule, huku akiongezea kuwa shule nyingi hufanya vibaya kutokana na siasa duni kutoka kwa wazazi na wanakijiji.

Kwa upande mwingine, Maangi aliwashauri wazazi kuwekeza katika elimu ya wanao, ili waje kujisaidia na kujitegemea katika siku sijazo.

“Siku hizi hakuna kitu kingine mzazi anaweza kumfanyia mwanawe kama sio kumsomesha ili asije kuwa mzigo kwako,” alisema Maangi.

“Kwa hivyo nawaomba wazazi kuwekeza katika watoto wenu ili wajitegemee na kuchangia kimarisha uchumi wa kaunti ya Kisii na nchi kwa jumla,” aliongezea Maangi.

Aliongea mnamo siku ya ijumaa katika shule ya wavulana ya Riokindo inayopatikana katika wadi ya Bokimonge eneo bunge la Bomachoge Borabu, wakati wa kupeana zawadi kwa wanafunzi waliofanya vyema katika mtihani wa kidato cha nne cha mwaka wa 2014.

Maangi aliwapongeza waalimu na wazazi wa shule hiyo kwa ushirikiano walio nao uliopelekea shule hiyo kuandikisha matokeo ya kuridhisha, ambapo aliwaomba kuendelea na ushirikiano huo ili kuinua viwango vya masomo katika kaunti ya Kisii.

Naibu gavana aidha alisema kuwa serikali ya kaunti itaweka kitita cha shilingi million tano katika makadirio ya bajeti ya mwaka wa 2016/2017, ili kuwasaidia wanafunzi wanaotoka familia maskini kupata elimu.

“Serikali yetu ya kaunti iliongeza pesa za ustawi wa wadi kutoka shilingi milioni moja katika mwaka wa 2014/2015 hadi million tatu katika makadirio ya bajeti ya mwaka huu na tumeahidi kuongeza pesa hizo hadi milioni tano katika kila wadi ili kuwasaidia wanafunzi wasiojiweza kugharamia elimu yao,” alidokeza Maangi.