Kasisi wa kanisa ya katholiki katika chuo cha Kisii Lawrence Nyaanga ameomba kanisa zote kushirikiana na kupiga vita dhidi ya madawa ya kulevya katika jamii.
Akiongea leo, Jumatano katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kisii wakati shirika la Kupambana na madawa ya kulevya nchini NACADA lilipoanzisha mafunzo na fahamisho juu ya hatari ya madawa za kulevya, Nyaanga aliomba kanisa zote kushirikiana kwa pamoja ili kufunza wakaazi kuhusiana na madhara ya madawa ya kulevya.
“Naomba kanisa zote katika kaunti yetu ya Kisii kuwa za kwanza kuhubiri kuhusu madhara ya madawa ya kulevya katika jamii na jinsi mtu anastahili kujiepusha na matumizi ya madawa hayo,” alihoji Nyaanga .
Aidha, alisema kuwa wameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa watu, hasa wanafunzi wa chuo cha Kisii na vyuo vingine katika mji wa Kisii wamefahamishwa vyema jinsi ya kupambana na madawa hayo ya kulevya.
Shirika la kupambana na madawa ya kulevya, NACADA, likishirikiana na chuo kikuu cha Kisii walianzisha kampeini ya siku tatu, huku leo na kesho ikiwa ni mafunzo, na siku ya ijumaa itakuwa ni kupita katika barabara za mji wa Kisii ili kuwafahamisha na kuwaelimisha wakazi juu ya hatari ya madawa ya kulevya, huku mwenyekiti wa shirika hilo John Mututho akitarajiwa kuhudhuria hafla hiyo.
Kulingana na shirika hilo, watu wakipewa mafunzo jinsi ya kujiepusha na utumizi wa madawa hayo, wengi watajiepusha, na hilo ndio lengo lao kama shirika.