Wahudumu katika makao ya watoto mayatima ya Swabur Orphanage Home eneo la Kisauni, Kaunti ya Mombasa, wanaomba msaada kutoka kwa wahisani baada ya makao hayo kuathiriwa na mafuriko.
Hali hiyo ilisababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Jumapili na kutatiza shughuli eneo hilo.
Iliwalazimu wahudumu wa kituo hicho kuhamisha watoto hao wapatao 80 hadi katika nyumba mbadala huku mali yenye dhamani ikiharibiwa na maji ikiwemo chakula na vifaa vya kulalia.
Akizungumza na mwandishi huyu alipozuru eneo hilo siku ya Jumapili, mwanzilishi wa kituo hicho Bi Zaharia Mwalimu, alisema kuwa wanahitaji msaada wa kuondoa maji hayo yaliyojaa katika nyumba hizo.
“Tuliletewa mashine ya kutoa maji lakini haikuondoa maji yote. Bado maji ni mengi na hatujapata msaada wowote,” alisema Bi Mwalimu.
Mwalimu aliongeza kuwa kwa sasa kituo hicho kinakumbwa na uhaba wa chakula na pia tishio la kupata maradhi ya kipindupindu ikizingatiwa kwamba watoto wengi bado ni wachanga.
Wahudumu hao wanalaumu viongozi wa eneo hilo kwa kukosa kutafuta suluhu la kudumu kuhusu mafuriko hayo, kwa kuwa kila kunaponyesha hali hiyo hujirudia.
“Kila kukinyesha huwa kunashuhudiwa mafuriko. Tunaomba viongozi wetu angalau watuchimbie mitaro ya kupitisha maji kwa sababu tumechoka na tatizo hili,” alisema mkaazi.