Katika juhudi za kuhakikisha kila mwanafunzi anafaidi na ubora wa elimu nchini, mkurugenzi mkuu wa Huduma za Maktaba Kenya ameahidi kushawishi serikali kujenga maktaba kila eneo bunge.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiwa katika ziara ya kupokeza vitabu katika shule ya upili ya Nyamuya ilioko eneo Bunge la Bobasi, mkurugenzi huyo Bwana Samuel Nyangeso, alizungumzia umuhimu wa uwepo wa maktaba kila eneo bunge kuwa itawafaa si tu wanafunzi, bali wote wanaopenda kujiendeleza kimasomo.

“Ningependa kuona kila mwanafunzi akifaidi, na naiomba serikali izingatie kuweka na kujenga maktaba mbili kila maeneo ya bunge,” alisema Mkurugenzi.

Aidha, Nyangeso aliwaomba wanafunzi wote kuchukua nafasi yao kudurusu vitabu na kuepuka kutumia mkato katika maswala ya masomo ambapo, alionyesha maskitiko yake kuhusu kudidimia kwa utamaduni wa masomo miongoni mwa vijana wa wakati huu.

Bwana Nyangeso hakusita kuwapongeza walimu na wote wanaochangia katika kukuza maendeleo ya elimu, ambapo hasa eneo hilo ambalo alidokeza kuwa limeanza kuimarika kwa siku za hivi karibuni.

Mkurugenzi huyo aliwasilisha mchango wa vitabu wa jumla ya shilingi elfu mia mbili kwa shule hiyo.