Chuo kikuu cha Kisii kimejitolea kupigana na utumizi wa pombe haramu na dawa za kulevya kupitia vituo vyao vya ushauri nasaha na makundi ya marika kwenye chuo hicho ambayo yamejikakamua kung’oa uraibu huo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mmoja wa wahadhiri wakuu wa chuo hicho akiongoe siku ya Ijumaa baada ya kukamilika kwa kampeni ambayo iliandaliwa kwa siku tatu wiki jana alisema kuwa wamehakikisha kuwa kila kitengo cha taaluma mna makundi maalumu ambayo yanajihusisha na ushauri kwa wenzao ambao wanaonekana kuwa wanafuata mkondo potovu.

Joseph Mairuthi ambaye pia alimwakilisha Chansela Mkuu wa chuo hicho Prof. John Akama ambaye alisemekana kuwa nje ya nchi kwa shughuli rasmi, alifafanua kuwa chuo cha Kisii ni kimojawapo miongoni mwa vichache ambavyo vimekuwa katika mstari wa mbele kuhubiri  umuhimu wa kuacha utumizi wa pombe, na kuepukana na matumizi ya mihadarati.

Profesa Mairuthi alimshukuru mwenyekiti wa baraza kuu la Kenya la kupigana dhidi ya mihadarati (NACADA) John Mututho kwa kuwahakikishia ujenzi wa kituo cha urekebishaji tabia na matibabu kwa waathiriwa, na kumtaka kuendelea na mkazo huo ili kuona kwamba jinamizi hilo la dawa za kulevya limeangamizwa kote nchini.

Kampeni hiyo iliwaleta wanafunzi kutoka taasisi mbali mbali za elimu kutoka katika kaunti ya Kisii ambao walisaidia kusambaza ujumbe huo kwa wakaazi wa mji wa Kisii na viunga vyake.