Idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa imewataka vijana waliojitosa katika makundi ya kihalifu kujisalimisha kwa maafisa wa usalama la sivyo wakabiliwe kisheria.
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki amesema kuwa iwapo vijana hao watajisalimisha, basi serikali itawasaidia katika kujiendeleza kimaendeleo sambamba na kujikimu kimaisha huku akisisitiza kuwa usalama umeimarishwa Mombasa.
Kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Achoki alisema kuwa maafisa wa usalama wametumwa katika kila sehemu katika kaunti hiyo kuhakikisha kuwa wanaimarisha usalama na kuonya kuwa atakayejaribu kuzua vurugu atakabiliwa kwa mujibu wa sheria.
Wakati huo huo, kamishna huyo aliwahimiza viongozi mbalimbali wa kisiasa, kidini na jamii kwa jumla kuhakikisha kuwa wanawashauri vijana hao kujitenga na maswala ya kihalifu ili kuhakikisha kuwa wanadumisha usalama katika Kaunti ya Mombasa.
"Tunawaagiza vijana waliojiunga na uhalifu kujisalimisha mara moja. Serikali itawasaidia kujiendeleza kimaendeleo lakini watakaokaidi watakabiliwa kisheria. Ningependa pia kuwaomba viongozi kuhakikisha kuwa wanawashauri vijana vizuri,” alisema Achoki.
Kwa upande wake, afisa mkuu wa baraza la viongozi mbalimbali wa kidini katika eneo la Pwani Kasisi Stephen Anyenda, alisema kuwa baraza hilo litashirikiana kwa karibu mno na idara ya usalama kuhakikisha kuwa Kaunti ya Mombasa na eneo zima la Pwani liko salama.