Afisa wa kikundi cha Vijana katika Kaunti Ndogo ya Subukia Leah Ng’ang’a ameweka wazi kuwa makundi yanayopokea mikopo kutoka kwa hazina ya Uwezo yatalipa pesa hizo na kuondoa dhana kuwa huenda mikopo hiyo haitalipwa.
Akizungumza siku ya Jumamosi katika kituo cha kibiashara cha Kabazi kwenye hafla ya kutoa hundi kwa makundi 18, Afisa huyo alisema kuwa kuna Maafisa ambao wanatembelea makundi hayo na kutoa ushauri na kuhakikisha wanalipa mikopo yao ipasavyo.
“Bodi ya kitaifa ya hazina ya Uwezo imeweka mikakati kabambe ya kufuatilia vile makundi ya Vijana na wanawake katika eneo Bunge la Subukia yanavyotumia mikopo waliyopokea na pia kuhakikisha inalipwa kwa wakati,” alisema Ng’ang’a.
Naye Mwenyekiti wa hazina hiyo katika eneo Bunge hilo John Wanjiku alisema kuwa kufikia sasa takriban Sh15 milioni 15 zimetolewa kwa makundi ya vijana na wanawake 170 katika awamu ya kwanza na ya pili.
Mwenyekiti huyo alitilia mkazo kwa makundi hayo kulipa pesa hizo ili ziweze kunufaidi makundi mengine ambao pia wanahitaji kupewa mikopo na hazina hiyo.
“Lengo la Serikali ni kuwezesha wananchi kupigana na ufukara katika jamii kipitia hazina kama ya Uwezo. Namsihi kila mmoja kuchukua jukumu la kuhakikisha lengo hili limeafikiwa,” alisema Wanjiku.
Kaunti ya Nakuru imepokea kiasi cha takriban Sh191 milioni ambazo zimesambazwa kwa makundi katika maeneo Bunge yote 11.