Shule ya upili ya Kanunda, iliyoko eneo bunge la Kitutu chache kusini kaunti ya Kisii ilivamiwa usiku wa kuamkia leo na wezi, ambao walipora mali ya mamillioni ya pesa.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne katika shule hiyo, mkuu wa shule Edward Ouko alisema shule yake ilivunjwa usiku na wezi waliojihami na silaha za aina mbalimbali kama vile panga na shoka, kama alivyofahamishwa na mlinda lango wa shule hiyo.

Mlinda lango huyo alikamatwa na kufungiwa ndani ya darasa moja na wezi hao, kabla ya kutekeleza wizi wao jinsi walipanga.

Wakati huo huo, mkuu huyo alisema tarakilishi nyingi ziliibiwa, pamoja na mitambo mingine, kuisababishia shule hiyo hasara ya kiwango kikubwa.

“Hawa wezi walikuja wakamshika mlinda lango na kumfunga kamba huku wakimfungia ndani ya mojawapo ya darasa na kumwagiza kutopiga nduru pamoja na simu na kumtishia kuwa akipiga nduru angeuawa,” alisema Ouko.

Aidha, uchungunzi umeanzishwa kuhusu wizi huo, lakini kufikia sasa hakuna mshukiwa hata mmoja ambaye ametiwa mbaroni.

Kwa upande mwingine, wakaazi wa eneo hilo walio karibu na shule hiyo walilaani wizi huo, huku wengi wakisema ni njama ambayo ilipangwa kutoka hapo mbeleni na baadhi ya watu wasiojulikana.

“Shule hii yetu inastahili kuwajiri walinda lango zaidi ya watatu maana huyu mmoja angeuawa bila kujua jinsi alifariki, lakini Mungu alimuokoa kutoka mikono ya wezi hao,” alihoji Markus Gitebi, mzazi wa shule hiyo, na pia mkaazi wa eneo lililoko karibu na shule hiyo.