Mama mmoja katika eneo la Shika Adabu, Likoni, anadaiwa kumuua mwanawe wa kike mwenye umri wa miaka tisa usiku wa kuamkia siku ya Alhamisi, ili kupata fursa ya kuolewa.
Inadaiwa kuwa mama huyo, ambaye alikuwa amekosana na mumewe na kuanza uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwingine, alitekeleza kitendo hicho baada ya mchumba huyo kumwambia kuwa hawezi kumuoa kwa vile ana mtoto.
Akidhibitisha tukio hilo siku ya Alhamisi, Mkuu wa Polisi katika eneo la Likoni Willy Simba, alisema kuwa mama huyo kwa sasa anaendelea kuzuiliwa katika Kituo cha polisi cha Likoni huku uchunguzi ukiendelea.
Aidha, OCPD huyo alikashifu kisa hicho na kukitaja kama cha kinyama, kwa kusema kuwa haiwezekani mama mzazi kumtoa uhai mwanawe kisa na maana kutaka kuolewa na mwanamume mwingine.