Mahakama moja ya Nakuru imeagiza mshtakiwa anayedaiwa kuwa mwenye umri wa miaka 17, anayekabiliwa na shtaka la wizi kufanyiwa uchunguzi hospitalini kubaini iwapo huo ni umri wake kamili.
Hii ni baada ya mshtakiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumanne, kwa madai ya kumwibia Faith Nduati, jozi mbili za viatu, zenye thamani ya Sh6,000 tarehe Oktoba 26, 2015 katika eneo la Mbaruk, Kaunti ya Nakuru.
Hata hivyo, waliokua mahakamani walisalia vinywa wazi baada ya mamake mshtakiwa kutoa ushahidi dhidi ya mwanawe, huku akiarifu mahakama kwamba amelemewa kabisa na mtoto huyo aliyedai kwamba ana tabia mbaya.
Kutokana na hilo, alidai kwamba tabia hiyo ya mwanawe imempelekea kushindwa kukaa naye kwenye boma moja.
Licha ya hayo, Nyamirimba alikana shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkuu Doreen Mulekyo.
Hakimu Mulekyo aliagiza ripoti ya daktari ya kubaini umri wa mshtakiwa na iwapo ana matatizo ya kiafya iwasilishwe mahakamani Novemba 10, 2015 kesi hiyo itakapoendelea.