Mwenyekiti wa Shirika la wanawake la Women Grassroot Empowerment and Gender Equity, Grace Kibuku, ametaka wanaosusia kuchukua vitambulisho vya kitaifa watambuliwe ili suluhu litafutwe endapo kuna tatizo linalowapelekea kutochukua vitambulisho hivyo.
Akizungumza kwenye mahojiano na wanahabari mjini Njoro siku ya Jumatatu, Kibuku alisema idadi kubwa ya vijana wasiokuwa na vitambulisho ni dhihirisho kuwa hawapati huduma muhimu zinazotolewa na serikali.
Kutokana na hilo, amewahimiza wote waliohitimu umri wa miaka 18 kuhakikisha kuwa wana vitambulisho vya kitaifa ili wapate huduma hizo.
‘Hatua hiyo ni kuonyesha kuwa hawapati huduma muhimu za serikali kwa sababu hawawezi kufurahia huduma hizo ikiwa hawana vitambulisho. Ninawahimiza watu wote, hata wale ambao wamepoteza vitambulisho vyao kuchukua vitambulisho vya kitaifa,” alisema Kibuku.
Aliongeza: “Vitambulisho hivyo vinatolewa bila malipo yoyote na serikali ya Kenya. Kama kuna wale wanaokataa kuchukua vitambulisho hivyo, inafaa ijulikane kwa sababu hiyo ni haki yao.”
Grace Kibuku ambaye pia alikuwa akiwania kiiti cha mwakilishi wa wanawake kwenye kaunti ya Nakuru katika uchaguzi mkuu uliopita alisema huenda ukosefu wa vitambulisho miongoni mwa vijana unatokana na tatizo katika uongozi.
“Tunaona kuna shida katikia uongozi kwa sababu kitambulisho ni stakabadhi ya serikali inayotumika kujitambulisha. Ukiingia katika afisi yoyote, ni sharti uwe na kitambulishi cha kujitambulisha. Hata ukienda katika benki, ni lazima uwe na kitambulisho. Inamaanisha kwamba wachache ambao hawana vitambulisho vya kitaifa hata hawana kura. Hili ni jukumu la machifu na manaibu wao,” aliongeza Kibuku.
Kwa sasa, ametaka mamlaka husika kubaini kinachopelekea baadhi ya watu kutochukua vitambulisho huku akitoa wito kwa viongozi husika wakiwemo waandishi wa habari kusaidia katika kutatua shida hiyo.
“Tatizo liko wapi? Ni changamoto gani inazuia watu kupata vitambulisho vya kitaifa? Wanahabari pia wanaweza kufanya uchunguzi wao kwa vile ni muhimu kwa wtu kuwa na vitambulisho vya kitaifa pamoja na kura,” alisema Kibuku.