Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mamlka ya mpito nchini TA, imeonya kuwa ukosefu wa utekelezaji wa ugatuzi kikamilifu huenda ukazua rabsha nchini.

Aidha, mamlaka hiyo imesema kuwa Ugatuzi ni mfumo mzuri wa uongozi kwani maendeleo yanayoletwa na mfumo huo ni mengi.

Akizungumza siku ya Jumatatu baada ya kumalizika kwa warsha ya wiki moja ya maafisa wa mamlaka hiyo katika hoteli moja mjini Naivasha, Mwenyekiti wa TA, Kinuthia Wamwangi, alisema kuwa kaunti zinapata mabilioni ya pesa kutokana na mbinu zao za uwekezaji, hatua ambayo imeletwa kutokana na ugatuzi.

Huku muhula wa mamlaka hiyo ukimalizika Ijumaa wiki hii, Wamwangi alisema kuwa wanapanga kuondoka ili kuwachia bodi mpya usukani.

“Tunachukua fursa hii kuwaambia Wakenya kwaheri na kuwashukuru kwa namna ambavyo wamekuwa wakitupiga jeki, kwa sababu kama inavyodhihirika, ugatuzi umefaulu na ni kutokana na juhudi hizo,” alisema Bw Wamwangi.

Kwa mujibu wake, shughuli ya kuondoka ilianza miezi minane iliyopita na sasa walikuwa wakiandika ripoti kuhusu kazi ambayo wamekuwa wakiifanya ili kuiwasilisha kwa serikali kuu.