Mamlaka inayosimamia raslimali za maji nchini 'Water Resource Management Authority' (WRMA), imezindua kongamano la uimarishaji wa maji na raslimali kama njia moja wapo ya kuwawezesha wadau mbalimbali kufahamu umuhimu wa utumizi wa maji nchini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo nchini mhandisi John Olum amesema kuwa tamaduni za kale zimechangia kuwepo kwa changamoto nyingi katika sekta hiyo, na kuahidi kushirikiana na wadau kukabiliana na changamoto zilipo kwa sasa.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Olum alisema kuwa mamlaka hiyo itazidi kuandaa makongamano kwa jamii na wadau wa sekta ya maji nchini ili kuhakikisha kuwa raslimali ya maji nchini inaangaziwa kwa ukamilifu.

Olum alisema kuwa tayari mamlaka hiyo inashirikiana na serikali za kaunti nchini kuhakikisha kuwa swala la maji linaangaziwa kwa undani.

Aidha, alisema kuwa sheria zinazotumika kwa usimamizi wa maji hazikandamizi wadau bali huhakikisha maji yanawafikia wakaazi hata wa mashinani bila changamoto.

"Tutapanga makongamano na wadau wa sekta ya maji kuhakikisha kuwa sekta hii inaboreshwa zaidi,” alisema Olum.

Kongamano hilo pia litaangazia changamoto zinazosababisha uhaba wa maji, udhibiti wa utumizi mbaya wa raslimili na jinsi ya kuboresha sekta ya maji nchini.