Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu Jackson Mandago amesema kuwa chama cha Jubilee kitahakikisha amani katika kaunti hiyo haswa wakati huu tunapoelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza siku ya Jumanne baada ya kufunguliwa kwa bunge la kaunti hiyo ili kurejelea vikao vyake, gavana huyo alisema kuwa chama cha Jubilee kinawajumuisha wananchi pasipo misingi ya kikabila.
"Tunapoelekea mwaka wa 2017, sisi kama wanajubelee tutahakikisha amani kote nchini," alisema Mandago.
Mandago aidha aliwaonya wanasiasa dhidhi ya kuwagawanya wakenya kupitia vyama vya kisiasa vyenye misingi ya kikabila, na kudai kuwa vyama vidogo vidogo vinatumiwa kusambaza chuki na utengano nchini.
Hata hivyo, aliwarai wanachama wa chama pinzani cha Cord kuipa serikali muda wa kuwahudumia wananchi.
"Wanasiasa wengine waache mambo ya kutumia matanga kama njia ya kukuza sera zao na kutafuta uungwaji wa mikono," aliongeza gavana huyo.