Kanisa la Got Calvary Legion Maria katika eneo la Kisumu limeandaa maombi ya kufunga na kujitakasa kwa siku tatu kabla ya kufanya maombi ya amani kuombea taifa hapo jumapili.
Maombi hayo maalumu ambayo yanashirikisha kutubu na kukesha wakisali yataanza leo (Alhamisi) jioni kwenye kanisa la Mtakatifu Michael lililokp katika eneo la Ombeyi viugani mwa mji wa Kisumu.
Yakiongozwa na Askofu Mkuu wa kanisa hilo Jimbo la Kisumu Isaac Benjamin, maombi hayo yanatazamiwa kuleta amani na umoja miongoni mwa wakaazi wa eneo hilo pamoja na kumaliza nguvu za kishetani ambazo zimepagawa wanadamu wengi ambao wamegeuka kuwa ‘wanyama mwitu’ wakati wanapotekeleza maovu.
Akihitubu kwenye ibaada ya Jumapili katika makazi yake ya Kanisa la Mtakatifu Mary Immaculate lililoko mjini Kisumu, Askofu huyo Mkuu alitaka waumini kujitokeza kuhudhuria maombi hayo ambayo alisema kuwa yana umuhimu sana katika jamii ya kanisa na taifa hili kwa ujumla.
“Tunapomkimbilia Mungu hakika hatutaachwa milele. Naomba waumuni wajitokeze ili tumlilie Mwenyezi Mungu, muumba wetu ili aturehemu na atuokoe kutoka katika mkono wa adui na kutufungua minyororo ya shetani,” alisema Askofu Benjamin.
Kanisa hilo limekua kwenye mstari wa mbele katika kulilia amani ya Kenya, ambapo limekua likiandaa hafla za maombi maalumu kuombea amani ya nchi pamoja na kuhubiri umoja na utangamano miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.