Vingozi wa kidini na Wakaazi wa eneo bunge la Njoro waliandaa maombi maalum Jumatano mchana katika kituo cha biashara cha Njoro ili kuiombea na kuitakasa barabara ya Njoro kwedna Mau kutokana na kile walichokitaja ni uwepo wa mapepo katika barabara hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongozwa na Askofu Timothy Bii wa kanisa la African Inland, Vingozi hao wa kidini na wakaazi walifanya sala maalum ya kuitakasa barabara hiyo ambayo ni kati ya barabara hatari sana katika Kaunti ya Nakuru.

Akiongea wakati wa maomi hayo Askofu Bii aliwataka wakaazi kukoma kuwalisha mifugio wao pembeni mwa barabara hiyo kwani inachangia katika kusababisha ajali.

Vilevile aliwataka wazazi kuhakikisha kuwa wanawavusha wanao barabara kila wakati wanapotoka na kuelekea shuleni.

“Tumekuja hapa kumuomba Mungu kuondoa mapepo amabayo yamekuwa yakimaliza watu wetu kwa njia ya ajali katika barabara hii na bila shaka maombi yetu yatasikika. Lakini pia sisi kama watumizi wa barabara tuna jukumu la kuhakikisha kuwa tunapunguza hizi ajali kwa kukoma kuwalisha mifugo kando ya barabara na tusiwache watoto watembee barabarani peke yao,” alisema Askofu Bii.

Mwenyekiti wa wafanyi biashara katika mji wa Njoro Nicholas Kamiti naye alisema kuwa kama wakaazi wa Njoro wamejitolea kushirikiana na polisi katika kuwanasa madereva wanaokiuka sheria za trafiki, itasaidia pakubwa sana kupunguza idadi ya ajali barabarani akisema kuwa watawakamata madereva kama hao na kuwawasilisha kwa polisi.

“Tukiona dereva anaendesha gari kwa mwendo wa kasi ama anavunja sheria za trafiki sisi kama raia tutamkamata na tumpeleke kwa polisi. Nawasihi pia wakaazi wa hapa kuzoea kutumia vivukio vya barabarani vilivyojengwa ili tuzuie hivi visa vya ajali,” alisema Kamiti.

Mwezi jana Mbunge wa eneo hilo Joseph Kiuna aliwaongoza wakaazi katika kufanya maandamano ya kutaka maafisa wa polisi wa trafiki wa eneo hilo kuhamishwa kwa kile alichokitaja kuzembea kazini kufuatia engozeko la ajali katika barabara hiyo yenye shuguli nyingi.