Siasa ni mchezo uliosheheni ahadi tele.

Share news tips with us here at Hivisasa

Waliosomea sayansi ya siasa au wenye uzoefu katika ulingo huu hutumia mtego huu kistadi.

Wengi wa wanasiasa hudanganywa kwa kuelezewa mazuri watakayopata wakijiunga na chama fulani.

Rais Uhuru Kenyatta aliamua kutumia mbinu hii ya jadi katika ziara yake ya Pwani.

Rais Kenyatta alisema kuwa viongozi watakaowania vyeo mbalimbali kwa chama cha Jubilee watapewa vyeo serikalini iwapo watafeli kwenye mchujo.

Je hili litatimia?

Swali hili laweza kuwa kizungumkuti ikiwa tutafungwa na ufuasi usio na msingi.

Ufuasi wa aina hii unaweza linganishwa na hulka ya kondoo. Waweza anza kupigia upato mrengo wako wa siasa bila kudurusu historia ya siasa nchini?

Hili halitawahi timia kwa sababu nyingi sana.

Mojawapo ya sababu kuu ni idadi ya wale watakaobwagwa. Je, kuna nafasi ngapi za serikali ambazo watapewa?

Ikiwa utaweza kumbuka, baadhi ya sababu za talaka ya ndoa ya NARC ni kutotimizwa kwa ahadi.

Bwana Raila Odinga na wenzake walidai kwamba Rais mstaafu Mwai Kibaki hakutimiza makubaliano yao, baada ya kushindwa kugawana nadhifa serikalini.

Jambo hili pia linawakumba wanaJubilee na ni wazi kwamba haliondoki leo wala kesho.

Ikiwa walishindwa kugawana wizara kati ya vyama vya URP na TNA, watawezaje kuwatunuku waliokosa fursa?

Hii ni ndoto tamu ya mchana ambayo haiwezi timika.

Ahadi hii ni propaganda tupu itakayoua demokrasia na maono ya wanasiasa wengi kutoka Pwani.