Mwaka uliopita ulihitimika kwa misukosuko si haba; shukrani kwa Mwenyezi muumba mbingu na dunia na vyote vilivyomo tumeweza kuuona mwaka wa 2015.
Mojawapo ya swala lililokuwa la kizungumkuti kwa wote mwaka jana lilikuwa ukosefu wa usalama. Jitihada si haba zimehimarishwa kuleta hali ya utulivu na kuifanya nchi yetu mahala mwafaka kwa wazalendo kuendesha shughuli zao kikamilifu bila wahaka aidha kibuhuti.
Alipojiuzulu Inspekta wa Polisi David Kimayo, alitwikwa jukumu hilo Joseph Boinett la kuhakikisha kuwa usalama unarejeshwa, hatua ambayo inadhihirisha uwezo wa kukabili changamoto la ukosefu wa usalama.
Twangoja kuiona kazi aula ya Boinett itakayowarudishia wananchi ushujaa wa kutekeleza wajibu wao pasi na kutetereka.
Joseph Ole Lenku naye alibadilishwa na Joseph Nkaissery, ambaye pia ametudhihirishia kuwa anataka kila mwananchi awe na imani naye.
Sehemu ambayo itaangaziwa ni kuhakikisha kuwa mambo si yalivyokuwa, bali yanavyostahili.
Nitembeapo kote wanapotangamana wakenya nakutana na walinda usalama wanaokagua silaha hatari kama vile guruneti, baruti, bomu na zana nyinginezo za vita. Swali ambalo wengi tunajiuliza ni je, wanavijua vifaa hivi vinatumikaje? Hatua zipi za kuchukuliwa endapo zana hizi watazipata? Na je, walinda usalama wanazijua zana hizi za vita na uharibifu? Ni kweli kuwa Vifaa vinavyo tumiwa na wengi hapa vimeharibiwa.
Elimu mwafaka itolewe ili wananchi wajue namna ya kujizuia na vifo kiholela. Mafunzo kwa walinda usalama kuhusu vifaa hivi pia yanafaa, na zaidi ya yote, ijulikane kwa wote usalama ni mimi na wewe, sote tushirikiane kama kiko na digali kuhakikisha usalama dhabiti.