Utumiaji wa mihadharati na ukosefu wa ajira haviwezi kuendelea kuwa visingizio vya kukithiri kwa uhalifu.
Jamii inawajibu mkubwa wa kuhakikisha usalama unapatikana katika maeneo yaliyoathirika katika Kaunti ya Mombasa, kwa kuwalea watoto katika maadili yanayofaa na wala sio kuwatekeleza.
Katika siku za hivi majuzi, visa vya uhalifu katika mitaa ya Kisauni, Mshomoroni, Old Town na sehemu za Likoni vimekithiri kwa kiwango cha kutamausha.
Licha ya wakuu wa usalama katika kanda ya Pwani kuimarisha juhudi zao za kukabiliana na shida hii, bado magenge ya wahuni yanadaiwa kutowapa amani wakaazi katika sehemu hizo usiku na hata mchana.
Gavana wa Mombasa Hassan Joho alithibitisha kuwepo kwa magenge ya wahuni katika Mtaa wa Old Town, alipotoa hotuba katika sherehe za Eid Baraza.
“Wakati wa Ramadhan baadhi ya vijana walikuwa wakizunguka katika mtaa wa Old Town wakiwa wamejihami kwa visu, kwa nia ya kuwashambulia wakaazi,” alisema Joho.
Watu kadhaa wamelalamikia kuporwa mali zao, peupe kupigwa na hata wengine kupoteza maisha baada ya kujikuta mikononi mwa magenge haya.
Jamii zimechangia pakubwa uwepo wa magenge haya kwa kutoa mandhari shwari, yanayokidhi vitendo vyao haramu, huku baadhi ya wakaazi wakiwaficha wahalifu na pia kuwatetea baada ya kutekeleza uhalifu.