Ufisadi katika taifa la Kenya umetajwa kama janga la kitaifa, huku baadhi ya wizara mbalimbali zikipatikana kuhusika kwenye kesi za ufisadi.
Kwenye kisa cha hivi majuzi, aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Bi Ann Waiguru alijipata pabaya baada ya jina lake kupatikana katika orodha ya mawaziri waliodaiwa kujilumbikizia mali ya umma.
Kenya kama taifa huru ilibuni jopo maalumu la kukabiliana na visa vya ufisadi, chini ya Tume ya kukabiliana na ufisadi nchini EACC.
Jopo hilo lilipewa jukumu la kuwahoji na kuwafungulia mashata wakuu wa serikali wanaojihusisha kwenye visa ufisadi.
Hata hivyo, kufikia sasa hakuna kiongozi aliyetiwa mbaroni kwa kuhusika katika sakata za ufisadi.
Katika Kaunti ya Mombasa, hiyo imekuwa kinaya kikubwa kwani maafisa wa trafiki waliofanyiwa ukaguzi walipatikana kushiriki pakubwa kwenye visa vya ulaji hongo.
Naibu afisa mkuu wa trafiki eneo la Mtwapa Francis Abura alikuwa na wakati mgumu kueleza mtu aliyemtumia pesa zenye kima cha shilingi elfu tisini.
Kwenye rekodi ya Mpesa, Obura alipatikana kuwatumia wakuu wake katika eneo la Kilifi na Pwani kwa ujumla pesa mara kadhaa huku akijitetea kuwa zilikuwa za kuwasaidia baada ya wao kuomba msaada.
Kwa upande wake, Monicah Jebet afisa wa trafiki eneo la Voi, alionekana kumtumia mkuu wake pesa mara kadhaa wakati alipokuwa Kakamega. Afisa huyo pia alishindwa kueleza namna biashara ya mahindi aliyodai wanafanya na mkuu huyo inavyoendeshwa.
Ikiwa maafisa wa serikali wanajihusisha na visa kama hivyo, nani atakabiliana na ufisadi humu nchini?